SHENG' NA USANIFISHAJI WAKE
Nilishangazwa ajabu Profesa Kimani Njogu, Profesa Mukoma wa
Ngugi, Bi. Jane Obuchi na Kilolo Munyao waliposhabikia na kuwa makini
kusikilizi mwandishi wa Sheng’ Felix Omondi akiwasilisha tafsiri yake ya
kifungu cha bibilia tulichopewa kutafsiri wakati wa kongamano la Ituika agosti
12 mjini Naivasha. Pamoja na kwamba washiriki wengi walikuwa ama wandishi wa
Kiswahili au wapenzi wake ukumbi ulichangamka wakati Felix Omondi alikuwa
anatoa wasilisho lake. Binafsi sikutarajia kwani mara kwa mara jamii ya wapenzi
wa Kiswahili imetaja sheng’ kuwa maradhi katika makuzi ya Kiswahili. Baada ya
hapo tuliingia kwenye mjadala mkali ulioendelea hadi saa kumi asubuhi siku iliyofuatia. Majadiliano hayo yalihusisha
Paul Nganga, Dr. Maina Mutonya, Dr. Kuria na Dr. Dosline. Miongoni mwa mengi
yaliyojadiliwa ni wasilisho la Felix Omondi. Wanne hao walinifunza mimi jogoo
wa shamba mengi nisiyoyajua kuhusu Sheng'. Kwanza ni kuwa Sheng' huwa na
'lahaja' zake kwa kutegemea sehemu au eneo la chimbuko. Nilibaini kuwa Sheng'
hutofautiana kwa kutegemea kazi ya wanaobuni msamiati. Mfano kuna tofauti kati
ya Sheng' ya Makanga na ile ya Vijana wanaofanya kazi ya mjengo. Pia ilibainika
kuwa kuna Sheng' ya zamani na ya sasa miongoni mwa mengine. Hapa ndipo
ninapozua hoja yangu kuhusu usanifishaji wa Sheng'.
Ikiwa Sheng' itasanifishwa ili kusomwa kama lugha ya kwanza kwa watoto wanaotoka kwenye mitaa iliyosheheni lugha hiyo ni njia zipi zitakazotumiwa kuteua msamiati?
Baadhi ya vikwazo vinavyoweza kuzuia mchakato
huo vinatokana na :
- Msamiati wa lugha hii hubadilika kila mara. Huku kubadilika kunamaanisha kuwa lugha hii haina mizizi ya kuifanya iwe imara.
- Msamiati unaotofautiana kikazi, kiumri, kulingana na sehemu ya chimbuko na mengine ni ishara kuwa Sheng' haina usawa kwa wazungumzaji wake. Lugha yoyote lazima iunganisha jamii hata kimsamiati. Mfano hata ijapokuwa Luubukusu ya Bungoma mjini kitatofautiana na ile ya eneo kama Bumula, asilimia 98 ya msamiati ni sawa.
- Lugha hukua kutokana na kuongezwa kwa msamiati mpya. Hii ni tofauti na sheng' ambayo hubadilisha msamiati kila mara na kuutupilia mbali ule wa zamani.
- Isitoshe lugha huhusishwa na jamii husika. Mfano Luubukusu - jamii ya Baabukusu, Kiswahili - jamii ya waswahili, Ekegusii - jamii ya Wakisii... Je kuna jamii inayomiliki sheng'? Haya yakizingatiwa na kuchunguzwa kwa kina, huenda suluhu ya kusanifisha au kutoisanisha Sheng' itapatikana.
Mwisho binafsi sidhani kuwa kuharamisha au kuhalalisha
sheng' ni suala la kuamua haraka bila uchunguzi wa kina kwani lugha ni chombo
cha mawasiliano na sheng' hujaliza matakwa hayo.
Je unafikiri Sheng' ina nafasi katika mtaala mpya? Ni vipi msamiati wa Sheng' utasnifishwa?
Comments
Post a Comment